PICHA: Wazee wa Gabra katika eneo la Kalacha, North Horr.(Picha kwa hisani ya Medianorth.co.ke)
TAREHE 08/08/2018-Baadhi ya wazee kutoka jamii ya Gabra wameelezea kughadhabishwa na matamshi waliyodai yalitolewa siku mbili zilizopita na waziri wa maswala ya vijana na michezo katika kaunti ya Marsabit Umuro Roba Godana.
Wazee hao wanasema kwamba wamesikitishwa mno na kauli ya Umuro kwamba watu kutoka jamii ya Gabra waliuawa kinyama kila mara wakati wa uongozi wa aliyekuwa gavana wa jimbo hili Ukur Yattani.
Wameitaja kauli hiyo ya Umuro kama ya kuidhihaki jamii ya Gabra kwa jumla na wala si mtu binafsi.
Wazee hao wakiongozwa na aliyekuwa diwani wa Dukana Ali Adano wamemtaka waziri Umuro kukoma kuzungumza kwa niaba ya jamii ya Gabra wakidai kwamba hana mamlaka yoyote ya kuzungumza kwa niaba yao.
Badala yake wamemtaka afisa huyo wa serikali ya kaunti kuyatekeleza majukumu aliyopewa ya kuhudumia wananchi wa jimbo hili kama waziri kwa uadilifu mkubwa kama inavyotakina na kukoma kujihusisha na maswala ya kisiasa yasiyo na maana haswa ikizingatiwa msimu wa siasa umepita.
Akizungumza na Radio Jangwani kwa njia ya simu waziri Umuro amejitenga na madai yaliyoibuliwa na wazee hao akisema hakusema jambo kama hilo.
Matamshi hayo yanadaiwa kutolewa kwenye ziara ya Gavana wa jimbo hili Mohamud Ali eneo la Dub Goba viungani mwa mji huu.
Wazee hao wametoa wito kwa wenyeji wa jimbo hili kuzika tofauti za kisiasa na badala yake kukumbatia maridhiano na kuungana kwa ajili ya maendeleo.
Kwingineko wazee hao kutoka jamii ya Gabra wametoa wito kwa idara za afya ya umma na ile ya mifugo katika serikali ya kaunti, kuchukua hatua za haraka kukabili magonjwa ya Kalazaar, homa ya Rift Valley pamoja na ugonjwa wa nagana unaosababishwa na ndorobo ama ukipenda tsetse fly kwenye maeneo yaliyotambulika kuathirika.
Wameeleza kwamba mamia ya mifugo wao tayari wameangamia hususan katika maeneo ya Gas kwenye wodi ya North Horr na maeneo mengine jimboni kutokana na ugonjwa huo wa nagana.
Wameiomba serikali kuwatuma wataalam katika maeneo yaliyotambulika kuathirika kukadiria hali.
Wameitaka serikali kutekeleza zoezi hilo kwa usawa.