PICHA: Wanafunzi wa shule msingi ya Tigo na wafadhili wao PACIDA, Kaunti ya Marsabit.
TAREHE10/08/2018-Wito umetolewa kwa wanaMarsabit kujitenga na chuki, ukabila na siasa potovu na badala yake kuwajengea watoto mazingira bora ya amani.
Akizindua rasmi warsha ya amani baina ya shule za msingi katika shule ya msingi ya Tigo, naibu kamishna wa kaunti ndogo ya Chalbi Stephen Kavulu amesema jamii inawajibu wa kuwajengea watoto uwezo wa kujitambua katika umri mdogo kuwasaidia kukuza amani.
Kwa upande wake afisa mkuu wa elimu katika wadi ya Sololo Abdulai Dida amepongeza shirika la PACIDA kwa wazo la kuwashirikisha watoto kwa maswala ya amani, akisema itasaidia pakubwa kujenga msingi bora kwa vizazi vya kesho kujivunia amani na maendeleo.
Amesema shule takriban kumi katika maeneo hayo tayari yamehusishwa kwenye mpango huo, akiongeza kuwa kuna haja ya mikakati zaidi kuwekwa kuhusisha shule zaidi kwenye maswala ya amani.
Mratibu wa mpango huo wa elimu ya amani katika shirika la PACIDA Guyo Diba amesema kupitia mafunzo watakayopata watoto hao watakuwa mawakala wakuu wa amani, kwa kupitisha ujumbe huo kwa wazazi wao na wanafunzi wenzao.
Amesema mpango huo umelenga jamii za wodi za Turbi na Sololo kukumbatia amani na maridhiano.
Amesema elimu ya amani inafaa kujengwa mapema sana ili kila mtoto aone ana fursa ya kutekeleza katika kukuza amani.
Ameongeza kuwa warsha hiyo itawapa watoto fursa ya kutangamana na kubadilishana mawazo kuhusu si amani tu bali pia ndoto na malengo yao, kando na kuwapa nafasi ya kushiriki michezo na maonyesho mbalimbali.
Hafla hiyo ya siku tatu imedhaminiwa na shirika la PACIDA.
Aidha, hafla ya uzinduzi imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa elimu pamoja na wa kiutawala kutoka kaunti ndogo za Sololo na Turbi.
Kauli mbiu ya warsha hiyo ni “Mimi sio mtoto tu, mimi ni mkuzaji wa amani”