PICHA: Wakaazi wa kijiji cha kubibagasa wakipokea dawa hizo ya Rift Valley Fever.
TAREHE 08/08/2018-Zaidi ya familia 100 katika kijiji cha Kubibagasa kilichoko lokesheni ya Dirib Gombo kwenye wadi ya Sagante/Jaldesa wamepata msaada wa dawa za kuzuia homa ya Rift Valley, kando na kupokea uhamasisho wa kitaalam kuhusiana na matumizi ya dawa za kuzuia mbu kutoka idara ya Afya jimboni.
Dawa hizo ni za kunyunyiza nyumbani na kupaka mwilini,ili kusaidia kuzuia mbu wanaoambukiza homa ya Rift Valley.
Wakaazi wa sehemu hiyo wameeleza matumaini yao kwamba dawa hizo zitawasaidia pakubwa, kukabili hofu iliopo wa kuenea kwa homa ya Rift Valley ambayo iliripotiwa sehemu hiyo.
Msimamizi wa idara ya afya katika kaunti ndogo ya Saku Gobba Boru, amebaini kuwa uhamasisho huo umejiri miezi kadhaa baada ya mtu moja kupoteza maisha kufuatia maambukizi ya ugonjwa wa Rift Valley eneo hilo.

Gobba ameeleza kwamba idara ya afya itaendeleza zoezi la kuelimisha umma kuhusu ugonjwa huo.
Ametoa wito kwa yeyote anayehisi dalili za ugonjwa huo hususan maumivu mwilini, kutembelea kituo cha afya kilicho karibu ili kuchunguzwa na pia kupata ushauri kutoka kwa mhudumu wa afya.
Naye mwakilishi wadi ya Sagante/Jaldesa Sora Katelo ambaye aliandamana na maafisa wa matibabu kutoka idara ya afya waliozuru eneo hilo, amesema madhumuni ya uhamasisho huo ni kuwapa wananchi elimu ya kutosha kuzuia uwezekano wa maafa zaidi kutokea.
Wakati huo huo Sora ameeleza kuwa vyandarau 300 vya kuzuia mbu viko tayari kusambazwa,ili kuwafaidi akina mama wajawazito katika juhudi za kuzuia magonjwa yanayosambazwa na mbu.