PICHA: Kamishna ya kaunti Marsabit Gilbert Kitiyo akihutubia wanahabari katika afisa yake.
06/09/2018-Watu wawili wamedhibitishwa kuuwawa kufuatia mapigano yaliyozuka baina ya jamii mbili eneo la Horender, eneo bunge hili la Saku.
Kamishna wa kaunti ya Marsabit Gilbert Kitiyo amesema mtu mmoja aliuwawa jana jioni wakati wawili wakijeruhiwa kwenye shambulizi hilo.
Kulingana na Kitiyo, mapigano hayo yalizuka baina ya wanavijiji wa Horender na Kubi Kalo kutokana na swala la makaazi, kuhusu idadi ya watu na mifugo watakaoruhusiwa kuhamia sehemu hio sawia na swala la maji.
Kwenye shambulizi la kulipiza kisasi,mapema leo polisi wa akiba aliuwawa huku wawili wakijeruhiwa.
Kamishna Kitiyo amesema kwa sasa wanachunguza iwapo bunduki za polisi wa akiba NPR zilitumika kutekeleza uhalifu huo, na kwamba iwapo itadhibitishwa basi idara hiyo haitakuwa na budi ila kuchukua hatua za kurejesha bunduki zote zilizopo maeneo hayo.
Amesema wameweka mikakati kabambe kuzuia kuenea kwa mashambulizi hayo hadi hapa mjini Marsabit.
Aidha, ameongeza kwamba wanashuku mashambulizi hayo huenda yamechochewa kisiasa, na kwa maana hiyo idara hiyo itaandaa kikao cha dharura na viongozi wa kisiasa kutoka maeneo husika.
Ametoa onyo kali kwamba hakuna atakayesazwa iwapo itadhibitishwa amehusika kwa vyovyote vile na kuchochea wananchi kupigana.
Vile vile, ametoa wito kwa wananchi kutokubali kutumika na wanasiasa, ama mtu yeyote mwenye nia mbaya kuhujumu amani na kuleta uadui baina yao.