PICHA: Naibu wa rais William Ruto na viongozi kutoka kaunti ya Marsabit wakihuturia hafla ya kuchangisha pesa.
Tarehe 31-08-2018-Naibu rais William Ruto aliahidi kwamba serikali ya kitaifa itasaidia kununuliwa kwa mashine za CT Scan za hospitalini kwa gharama ya shilingi milioni 150 kabla ya kukamilika kwa mwaka huu.
Naibu rais alisema hili litasaidia kuwapunguzia wenyeji mzigo wa kusafiri safari ndefu kutafuta matibabu maalum hasaa ya saratani na ya figo. Ruto aliwaonya walimu wakuu wa shule za umma wanaowataka wazazi kulipa karo ilhali serikali imelipia tayari.
Alisema wanafunzi wote katika shule za msingi za umma na vile vile shule za upili za kutwa hawafai kulipa chochote. Aidha aliwaonya wazazi wanaowatuma watoto malishoni au kuwapa kazi nyingine nyumbani wakati wanafunzi wanafaa kuwa shuleni.
Ruto aliwataka wakaazi wa Marsabit kushirikiana na na serikali kuu katika kuafikia malengo ya ajenda kuu nne za Jubilee. Ameahidi kurejea Kaunti ya Marsabit katika kuzindua mpango wa kuwapa wenyeji maji safi akisema tayari kandarasi hiyo imepewa kampuni moja.
Ruto aidha amewashukuru wenyeji kwa kuunga mkono serikali ya Jubilee kwenye uchaguzi mkuu uliopita na kudumisha amani wakati huo.
Akizungumzia uteuzi wa waziri wa leba Ukur Yattani Ruto amesema uteuzi huo ulitokana na ahadi ambayo Jubilee iliweka wakati wa kampeni katika kaunti ya Marsabit.
Naibu rais amewataka wananchi pamoja na viongozi kuweka siasa kando na kuanza kushughulikia ajenda kuu za maendeleo.
Serikali ya kaunti imepewa ardhi ya hekari 200 za kupanua mji wa Marsabit baada ya gavana wa kaunti hii kuomba sehemu ya ardhi ya taasisi ya utafiti wa kilimo ya Kenya.
Ruto ameshutumu siasa za ukabila na kuwagawanya wakenya akisema Jubilee inahuribiri maendeleo. Mkutano wa Ruto umewaleta viongozi wote wa kaunti wakiwemo wabunge, seneta na gavana.
Gavana Mohamud Ali ameitaka serikali kutenga fedha zaidi kwa ajili ya kaunti hii ili kufanikisha miradi ya kaunti.
Gavana aidha ameweka wazi kwamba serikali yake imetenga shilingi milioni 69 za kuwasaidia wanafunzi waliokosa nafasi katika vyuo vikuu vya uma ili kufanikisha masomo yao katika vyuo vya kiufundi.
Viongozi wote wa kaunti hii waliohutubu katika mkutano wa naibu rais wameahidi kumuunga mkono naibu rais wakielekea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.