PICHA: Ukur na wenzake wakifuatilia kesi mahakamani hapo awali.


Aliyekuwa gavana wa Kaunti ya Marsabit Ukur Yattani ameondoa kesi aliyowasilisha mahakamani kupinga kuchaguliwa kwa Muhamud Ali kama gavana wa jimbo hili.

Baadala yake Ukur ameiachia wale walio na nia na kesi yenyewe kuendelea na kesi hiyo.
Aliyekuwa mwakilishi wa ubunge, wadi ya Turbi-Bubisa Pius Yattani amewasilisha nia ya kushiriki kwenye kesi hiyo.
Awali Pius Yattani aliiomba mahakama hiyo kumpa muda wa siku 4 kuweza kujiandaa kwa kesi hiyo.

Hata hivyo, hakimu Said Chitembwe aliitaka pande zote husika kuafikiana kuhusiana na namna ambavyo kesi hiyo itakavyoendeshwa hususan baada ya ombi la kujiondoa iliyowasilishwa na Ukur Yattani.


Amesema muda uliopo hauwezi ruhusu kesi hiyo kusongeshwa mbele zaidi.
Kufuatia maafikiano baina ya mawakili wote kwenye kesi hiyo, hakimu Chitembwe ameelekeza aliyewasilisha kesi hiyo ambaye ni Ukur Yattani, kutangaza rasmi kujiondoa kwake kupitia tangazo rasmi kwenye magazeti ya humu nchini kufikia Ijumaa hii tarehe 19 Jan, 2017.


Hatua hii itawapa walio na nia ya kushiriki kesi hiyo kufanya hivyo.

Aidha, mahakama itasikiza tena maombi ya kuondoa kesi iliyowasilishwa na Ukur na maombi ya kuendelea na kesi hiyo iliyowasilishwa na Pius Yattani Jumanne ijayo, tarehe 23.

Wahusika wengine kwenye kesi hiyo +ambao ni tume huru ya uchaguzi nchini IEBC na upande wa gavana wa sasa Muhamud Ali wametakiwa kuwasilisha majibu yao mahakamani kufikia Ijumaa hii tarehe 19.

Mwakilishi huyo wa zamani anataka kuhusishwa kwenye kesi hiyo hususan baada ya gavana huyo wa zamani kuteuliwa na rais Uhuru Kenyatta kuhudumu kwenye baraaza lake la mawaziri.

Duru zinaarifu kwamba Yatani alikutana na rais Uhuru Kenyatta hiyo jana kuandaa mazungumzo kuhusiana na swala la kesi hiyo miongoni mwa maswala mengine.
Kesi hiyo itasikizwa kwa ukamilifu tarehe 30 Jan hadi 3 Feb.

Hiyo jana mahakama ya Marsabit ilimpa Yatani, hadi hivi leo saa nane kuwasilisha uamuzi wake iwapo anataka kuendelea na kesi hiyo ama kuifutilia mbali.
Hata hivyo, uamuzi wa ombi la Yattani ya kuchunguzwa na kuhesabiwa upya kwa kura itatolewa Ijumaa hii, tarehe 19.

Yattani amewasilisha kesi mahakamani kupinga uchaguzi wa gavana Ali akidai hakuchaguliwa kwa njia ya uwazi na ukweli, na kwamba kura zake ziliibwa.