Waendesha bodaboda wameandamana leo hapa mjini Marsabit kulalamikia kile walichokitaja kama kuhangaishwa na maafisa wa trafiki.

Wamelalama kwamba katika muda wa wiki moja sasa wamekuwa wakitatizwa na maafisa hao ambao wanawakamata bila makosa.

Kando na hayo, wanabodaboda hao wanasema maafisa hao huitisha pesa nyingi kama faini.

Kulingana na wao wale ambao hawawezi kumudu faini hizo hunyanganywa pikipiki zao na kuzuiliwa.

Walionyesha ghadhabu zao kwa kuweka vizuizi barabarani pamoja na kuchoma magurudumu katikati ya barabara kuu hapa mjini Marsabit na kutatiza shughuli za kawaida kwa muda.
Wametoa wito kwa viongozi wakiongozwa na gavana Mohamud Ali, kuingilia kati na kutatua swala hilo kwa haraka.

Kulingana nao, kufikia sasa vijana karibia 50 wamekamatwa na kuzuiliwa, ama pikipiki zao kuchukuliwa na maafisa hao wa trafiki.

Aidha, wametoa wito wa kuondolewa mara moja kwa baadhi ya maafisa wa polisi waliowalaumu kwa masaibu yao.