Picha:Sr.Margaret Lekonon (Kushoto) akifuatilia misa takatifu kusherekea miaka 10 ya utawa katika Parokia ya Karare.
Mamia ya waumini wakubwa kwa wadogo hapo siku ya Jumamosi ya tarehe 17 Juni, wameungana na Sr. Margaret Kaimas Lokonon huku akisherehekea maisha ya ukristu ndani ya Miaka 10 ya kitawa. 
Sherehe hiyo ya kufaana iliandaliwa kanisa la Karare huku mahubiri ikiendeshwa na Mkurugenzi Mkuu wa Radio Jangwani na Kasisi Mkuu jimbo hili Padre Racho Ibrahim. 
Kwenye mahubiri yake Padre Racho amesema maisha ya Kitawa ni Maisha ya kujitoa zaidi kwa ajili ya wengine, kama mwanga unavyowaka ili wengine wafurahi na unapozima hauna faida kwa wanaopata mwanga huo ni sawa na masista ambao wanawaka kwa ajili ya kuhudumia jamii. 
Amempongeza Sr Margaret kwa kufikisha miaka Kumi akitumikia Kristu na kumtaka kuendelea kumtegemea Mungu ili aweze kutumikia zaidi na kufundisha jamii katika maisha ya kumtegemea Kristu. 
Aidha, amewashukuru wazazi wake kwa kukubali Sr Margaret kuitikia wito huo.
Amewapa changamoto wazazi kulea watoto wao ndani ya msingi bora wa Ukristu.
Sr Margaret ameelezea furaha yake akisema amejifunza mengi na kuvuka vikwazo vingi na kuvivumilia. 
Amewashukuru waumini jimboni na kuwaomba kuendelea kumkumbuka kwa maombi.  
Kadhalika, ameapa kukiri kuendelea kutetea maisha ya Ukristu.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na mapadre wa makanisa mbalimbali, watawa, jamaa ya Sr Margaret na waumini kutoka sehemu mbalimbali jimboni. 
Sr Margaret anahudumu katika Shirika la Masista la  Nirmala Dasi Sisters.
Yeye ni sista wa kipekee mzaliwa wa jimbo hili.