Picha:Mwanafunzi Huyu anarudi shuleni akitembea kando mwa barabara akiwa na hofu.
Wakaazi wa Marsabit wamelalamikia ujenzi mbovu wa barabara katika mji huu wa Marsabit wakisema haijafikisha kiwango kinachohitajika cha ubora kuweza kutumika na wananchi.

Wakaazi waliojawa na gadhabu wameandamana leo mchana hadi afisi ya barabara ilioko eneo la Bank Quarters hapa mjini Marsabit.
Akizungumza na Radio Jangwani mmoja wa waandamanaji hao, Stella Moraa ambaye anamiliki kliniki hapa Marsabit amesema kuwa kuna hatari kubwa ya kiafya kutokana na mikurupuko wa magonjwa akieleza kwamba mitaro ya kupitisha maji sasa imegeuzwa kuwa sehemu ya kutupa kila aina ya taka taka.
“Watoto wetu sasa wanalazimika kutembea kwa njia ya maji au mtaaro chafu wakitoka shuleni” Asema Stella.
Naye Mzee Said, Mkaazi wa eneo la Shauri Yako amehoji kuwa kila siku watu wanaumia katika mji huu wa Marsabit kutokana na kuanguka kwa mitaro akilaumu kujengwa kwa mitaro kiholela.
“Hivi Majuzi mwalimu mmoja ameanguka kwa mtaro akiwa anatembea huku akipiga simu na sasa amelazwa hospitalini baada ya kuvunjika mgongo” Asema Mzee Said.

Wakaazi hawa sasa wameiomba idara husika kushughulikia swala hilo wakisema pia hakuna pahala pazuri pa watu kutembea, mzunguko wa barabara ama(RoundAbout) na sehemu ya kuengesha Magari.